Wednesday, January 27, 2010
SAUTI ZA BUSARA ZAWIVA ZANZIBAR
Mwanamuziki mkongwe mwenye makazi yake ya kimuziki nchini Japan Fresh Jumbe akizungumza na waandishi wa habari mapema leo asubuhi kuhusu ushiriki wake pamoja na bendi yake nzima katika tamasha la sauti za busara
Hatimaye,kuna habari njema kutoka Zanzibari… Ukiachana na hali mbaya ya kiuchumi ya Dunia iliyoathiri bodi ya Utalii, na ukosefu wa umeme wa muda mrefu, tangu kati kati ya Disemba, hatimaye kuna mtazamo chanya juu ya Tamasha la saba la muziki la Sauti za Busara linalotazamiwa kung’arisha Zanzibar!
“Ni wakati mgumu sana tunajua, lakini juu ya sababu zote! lengo letu ni kusonga mbele, pamoja na Sauti za Busara”, Yussuf Mahmoud anasema, Mkurugenzi wa Busara Promotions. “Tamasha hili ambalo kauli mbiu yake mwaka huu ni MOTO ZAIDI litaleta watu pamoja katika kusherehekea, kuwasaidia vijana wenye uwezo wa kiutamaduni, kuwapa bahati ya kukutana na wasanii wakubwa katika jukwaa moja na kutoa fursa ya kubadilishana mawazo kutoka kwa mmoja kwenda kwa mwingine. Lakini si hivyo tu, Inaweza pia kuwa fursa ya kubadilishana uzoefu, kufahamiana na pia Tamasha la Sauti za Busara linatuwezesha kuboresha utalii mpya wa kiutamaduni nchini Tanzania.”
“Ni kweli”, tumedhamiria kuendelea, “kukosekana kwa umeme kisiwani imetuletea sote wakati mgumu, lakini tumejipanga na majenereta ya kutosha ili kuhakikisha mambo yote yanaendelea kama yalivyopangwa, usalama umeboreshwa na mpangilio mzuri kwa watazamaji. Ukiwepo umeme au ukikosekana, Sauti za Busara iko TAYARI!”
Labda tuwapashe tu kidogo kuwa; Toleo la saba la sauti za busara linaelekea kuleta “habari nzuri” kwa ajili ya Afrika, wasanii kutoka kona mbalimbali za Afrika wanajongea visiwani tayari kwa burudani. Hivi Mahoteli ndani ya mji mkongwe yamekwisha furika, wawezeshaji wa muziki duniani, wanautamaduni pamoja na waandishi wa habari kutoka pande mbali mbali za dunia wako tayari kuja pamoja kushuhudia nini kinaendelea katika mandhari nzuri ya muziki wa Afrika Mashariki.
Tofauti na miaka iliyopita, Sauti za Busara 2010 linakuja na vionjo adhimu, zaidi ya wanamuziki 400 watapanda jukwaa moja. Mbali na vikundi kumi na mbili kutoka Zanzibar na nane kutoka Tanzania Bara, Tamasha hili pia limeshirikisha makundi ishirini kutoka nje ya Nchi kama vile Kenya, Uganda, Afrika Kusini, Mozambique, Mayotte, Egypt, Guinea, Senegal, Gambia na Zambia.
Kama kawaida, tamasha hili hutokea kipindi cha sikukuu ya wapendanao hivyo kuongeza ladha zaidi. Kutoka viwanja vya watoto Kariakoo saa kumi kamili za jioni siku ya alhamisi tarehe kumi na moja februari kutakuwepo na maandamano makubwa na ya kipekee yatakayo ashiria ufunguzi rasmi wa tamasha hili la aina yake, wakiwemo wana sarakasi, mdundiko, ngoma na bendi, wote wakielekea Ngome Kongwe hadi itakapofika mida ya saa kumi na moja jioni. Kutoka hapo na kuendelea, kutakuwa na shoo za muziki kwa siku nne , pamoja na vikundi 40 (wanamuziki 400) akiwemo Thandiswa(Afrika Kusini), Nyota ndogo na Makadem (Kenya), Ba Cissoko (Guinea), Malick Pathe Sow (Senegal), Massar Egbari (Egypt), Banana Zorro, Fresh Jumbe, Chidi Benz (Tanzania) na wengi wengineo.
Kama kawaida, Tamasha huandaa mikutano na watu wajuzi mbali mbali na wasanii kwa mafunzo ya kiufundi kwa lengo la kuwawezesha watu kupata ujuzi kwa wapenzi wote wa muziki. Februari 16, kutakuwa na sherehe ya kumaliza tamasha zitakazofanyika Jambiani, muziki utakuwepo pamoja na ma DJ wa kimataifa kutumbuiza mpaka asubuhi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment