Tuesday, June 15, 2010

TAMASHA LA ZIFF


ZIFF NI NINI
Tamasha la Nchi Za Jahazi ( ZIFF ) ambalo linatimiza miaka 13 mwaka huu ni moja ya matamasha makubwa Afrika Mashariki na linatambulika duniani kote kwa kuinua na kuendeleza filamu, muziki na sanaa za kiafrika katika majukwaa ya kimataifa..

LINI NA WAPI LINAFANYIKA Julai 10-18, 2010 Kwa mwaka huu tamasha litaanza tarehe10 mpaka tarehe 18 ya mwezi wa saba(7), Kwa miaka mingi ZIFF imekuwa ikitumia Mji Mkongwe, hususani Ngome Kongwe kama jukwaa la matukio yote makubwa yanayotokea kwenye tamasha. Pia tamasha hufanyika katika mji wa Pemba na Tanzania Bara (Dar es Salaam na Bagamoyo).


ZAIDI KUHUSU ZIFF Tamasha la Nchi za Jahazi ni moja kati ya matamasha makubwa ya utamaduni kwa ukanda huu wa Afrika mashariki. Kwa miaka 13 sasa ZIFF kimekuwa chombo cha jumuia ya kizanzibari yenye malengo ya kuendeleza filamu za kiafrika na pia kusherehekea utajiri wa tamaduni tofauti kutoka ndani na nje ya Afrika.


FILAMU Kila mwaka ZIFF huleta pamoja maelfu ya watu toka hapa nyumbani, nje ya nchi, watengenezaji filamu toka Afrika na nje ya Afrika na wadau mbalimbali wa filamu kusheherekea tamasha hili la aina yake. Kwa miaka mingi sasa ZIFF imeweza kujijengea jina kutokana na maonyesho makubwa yenye kuvuta hisia za wengi na kufanikiwa kuendeleza na kukuza wigo wa sinema katika Afrika na ughaibuni pia.

Tunalitangaza tamasha kwa kupitia watu maarufu na wenye majina (Mfano tumeshakuwa na wasanii mbalimbali kutoka Hollywood ambao hualikwa maalum kama wageni rasmi) lakini tunajivunia uwezo wetu wa kujitolea katika kuendeleza na kutangaza vipaji chipukizi katika sanaa na filamu za humu nchini. UTAMADUNI Ingawa kwa asili tamasha ni la filamu, ZIFF tunaamini katika nguvu ya sanaa, Hivyo tumeandaa ratiba itakayosheheni pia wasanii wa muziki waliochaguliwa kwa umakini mkubwa kutumbuiza ambapo muziki utakua ukipigwa “live”. Pia kutakuwa na maonesho ya sanaa, mwaka huu kutakuwa na maonesho ya Vitenge vya Wax toka Uholanzi, Ghana, Congo na Tanzania tukijivunia sanaa ambayo sasa ni biashara kubwa duniani kote. JAMII Maendeleo na ushiriki wa jamii umekuwa changamoto muhimu kwa ZIFF. Tumeweza kuwashirikisha na kuwaleta wanafunzi na vijana hasa kutoka shule za msingi na sekondari, na kwa hivyo kuwawezesha kupata nafasi ya kuangalia filamu za Kiafrika na za Kimataifa. Kwa muda mrefu sasa Jukwaa la Wanawake ni jukwaa ambalo hujumuisha warsha na maonesho ya filamu ambayo hulenga kuendeleza majadiliano kuhusiana na shughuli za kijamii na haki za kisheria kwa wanawake. Vilevile jukwaa la wanawake huwapa fursa wanawake kujadili na kupanga mustakabali wao kama wanawake na pia kutambua uwezo na nafasi ya mwanamke katika kuendeleza jamii zao na zinazowazunguka. Katika kutambua uwepo na kuthamini vipaji vya watoto ZIFF, kwa kushirikiana na Taasisi ya Filamu ya Denrmark, huwaletea watoto programu inayolenga kuendeleza na kuhamasisha uelewa na utengenezaji filamu kwa watoto. SOKO ZIFF ni tamasha muhimu kwa wadau wa filamu duniani kwa kuwa mwenyeji wa mabaraza ya kuunganisha, kusambaza, kuendeleza na kutangaza filamu, hasa za Kiafrika, ZIFF inaendeleza usambazaji filamu kwa watengeneza filamu kutoka nchi zilizoendelea na nchi za Afrika kwa kuimarisha soko la filamu. MAFANIKIO YA MWAKA ULIOPITA 2009 Filamu ya Go With Peace Jamil (Afghanistan/Denmark) ambayo ilishinda tuzo ya SIGNIS na FIPRESCI mwaka jana iliweza kushinda pia katika tamasha la filamu la Goteborg baadae mwaka huo huo. Bilal ( ya Sourav Farangi) nayo ilishinda tuzo katika tamasha la IFF Las Vegas pamoja na Aljzeera Golden Award (Aljazeera IFF) Kaa tayari kwa filamu mpya zitakazozinduliwa mwaka huu ambazo HAUTAKIWI KUZIKOSA Tunayofuraha kuwatangazia filamu mpya zitakazotambulishwa rasmi mwaka huu. MOTHERLAND Uzinduzi filamu mpya ya Motherland (ENAT HAGER) iliyoongozwa na mtayarishaji mahiri Owen Ailk Shahadah ambaye ni Mshindi wa tuzo ya PAN- AFRICAN film festival 2010, Makala bora. MOTHERLAND ni filamu yenye mvuto inayogusa historia utamaduni na siasa ikisimulia hadithi mpya ya bara la Afrika ikiwa na wahusika kama vile Marais Meles Zenawi na Jacob Zuma na pia Mkufunzi maarufu Ali Mazuri na msanii Harry Belafonte. TWIGA STARS: TIMU YA MPIRA WA MIGU YA WANAWAKE TANZANIA. Kwa mapenzi na ushabiki mkubwa wa mpira wa miguu ambao unaonekana kukua kwa mwaka huu, ZIFF tunayo furaha kuwatangazia uzinduzi a filamu mpya ya TWIGA STARS, timu ya taifa ya wanawake ya mpira wa miguu ni filamu iliyoandaliwa na Nisha Ligon.
Filamu hii inayoonesha maisha ya Twiga Stars, timu ya mpira wa miguu ya wanawake Tanzania kwa mwaka mzima, inaonesha uchaguaji, kambi za mazoezi na ushiriki katika mashindano nje ya nchi pia matatizo yote wanayokutana nayo wasichana ambao wana ari, vipaji na shauku kubwa la kujaribu kuwa wachezaji mahiri wa mpira wa miguu katika moja ya nchi maskini duniani.

No comments: